Ijumaa, Septemba 29, 2017

Tshishimbi,Kamusoko wamtia hofu Lwandamina

Inachopiga hesabu Yanga ni kuwavaa Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi kesho.

Tayari ina uhakika wa kumkosa kiungo wake,  Mkongo, Pappy Kabamba Tshishimbi ambaye ana kadi tatu za njano lakini sasa imeingia katika hofu ya kumkosa kiungo wake tegemeo, Thabani Kamusoko baada ya Mzimbabwe huyo kupata dhoruba ndogo katika mazoezi ya jana.

Kocha  Mkuu wa Yanga, George Lwandamina raia wa Zambia, naye ameona ni vizuri kujipanga mapema, na tayari ameishachukua hatua.

Yanga wanatarajiwa kuvaana na Mtibwa Sugar, kesho Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Tshishimbi ndiye mchezaji wa kwanza kuondolewa kwenye mipango ya kocha wa timu hiyo, baada ya kupewa kadi ya tatu ya njano kwenye mechi iliyopita ya ligi kuu dhidi ya Ndanda FC iliyomalizika kwa timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0.

Kamusoko naye anatarajiwa kuukosa mchezo huo baada ya kupata majeraha ya goti na kutoka nje kwenye mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kamusoko akiwa nje anapatiwa matibabu, alimuomba daktari wa timu hiyo, Edward Bavu apumzike asiendelee na mazoezi kutokana na maumivu aliyokuwa anayasikia.

Mara baada ya Kamusoko kutoka, Lwandamina haraka akafanya maamuzi kwa kuwaandaa vijana wake wawili, Juma Makapu na kinda Maka Edward aliyepandishwa kikosi cha kwanza katika msimu huu wa ligi kuu ili wacheze namba sita inayochezwa na Tshishimbi ambaye ataukosa mchezo huo kutokana na adhabu hiyo ya kadi tatu za njano.

Lwandamina alionekana kuwandaa wachezaji hao kucheza namba sita baada ya Kamusoko aliyekuwa anatakiwa acheze namba sita mechi na Mtibwa kupata majeraha hayo na kulazimika kuwanoa vijana wake hao.

Wakati akiwaandaa wachezaji hao, katika mechi hiyo dhidi ya Mtibwa kocha huyo anatarajiwa kumtumia kiungo wake mpya, Pius Busitwa aliyekosa michezo minne ya ligi kuu kwa kukiuka kanuni za usajili kwa kusaini klabu mbili Simba na Yanga ambaye tatizo lake limemalizika.

Busitwa kwenye mechi hiyo, anatarajiwa kucheza namba nane iliyokuwa inachezwa na Kamusoko kwenye michezo iliyopita huku winga ya kushoto akianza kucheza Raphael Daudi.

Alipoulizwa Bavu kuzungumzia afya ya Kamusoko, alisema:

"Kamusoko amejitonesha goti lake aliloumia muda mrefu na kama ulivyoona ameshindwa kuendelea kwa ajili ya kumfanyia vipimo.

"Kikubwa kinachosababisha wachezaji wangu kujitonesha majeraha yao na wengine kupata majeraha mapya ni kutokana na hali ya uwanja ambao tunautumia, kiukweli ni mgumu lakini hatuna jinsi, inatubidi tuendelee kuutumia kwa sababu ndiyo uwanja tunaoutumia kuchezea mechi za ligi kuu," alisema Bavu.

BUNGE LATOA UFAFANUZI SABABU ZA KUCHUKULIWA GARI LA MBOWE NA KURUDISHWA NCHINI.



Ofisi ya Bunge imesema Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe hajanyang’anywa gari.

Taarifa iliyotolewa na Bunge  jana  Alhamisi imesema kilichotokea ni kwamba, gari hilo limerudishwa nchini ili dereva afuate utaratibu wa kupata kibali cha kusafiri nje ya nchi.

Mbowe yuko Nairobi nchini Kenya ambako Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anaendelea na matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Bunge limesema ni kweli gari lenye namba ya usajili STL 4587 aina ya Toyota Prado limetengwa maalumu kwa ajili ya kumuhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi na binafsi nchini.

“Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliomba gari ikamhudumie mjini Nairobi nchini Kenya na Ofisi ya Bunge iliridhia ombi hilo na kuomba taratibu zizingatiwe. Hata hivyo, ofisi iligundua kwamba gari ilikwenda Nairobi na dereva hakupata kibali cha kusafiri nje ya nchi ambacho kila mtumishi wa umma anayesafiri nje ya nchi lazima apate kibali hicho kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi,” imesema taarifa ya Bunge.

Bunge katika taarifa hiyo limesema kwa kuwa utaratibu haukukamilika, dereva aliambiwa alirejeshe gari hilo nchini na kuliegesha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha hadi utaratibu mwingine utakapokamilika.

“Dereva yupo Dodoma anakamilisha taratibu ili ofisi iweze kumuombea kibali Ikulu ndipo anaweza kurejea nchini Kenya kwa ajili ya kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,” imesema taarifa.

Ofisi ya Bunge imesema inasikitishwa kutokana na utaratibu unaotumiwa na Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa kuzungumzia masuala yanayohusu ofisi hiyo kupitia kwa msemaji wa chama kama inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa malalamiko kwa niaba ya ofisi hiyo.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kama ofisi nyingine zinazohudumiwa na Sekretarieti ya Bunge ambayo inapaswa kufuata kanuni na taratibu za uendeshaji wa Ofisi na ni kosa kwa mtumishi kwenda kinyume na masharti ya Utumishi wa Umma,” taarifa hiyo imesema.

Imeelezwa katika taarifa kuwa ni dhamira ya Ofisi ya Bunge kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma na zile za Bunge bila kuchanganya na siasa.

“Ofisi ya Bunge inauhakikishia umma kuwa taratibu zikishakamilika Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ataendelea kuhudumiwa popote atakapokuwa,” imesema taarifa hiyo.

HALOTEL TOENI HUDUMA ZOTE ZA MAWASILIANO VIJIJINI: KAMATI YA BUNGENI YA MIUNDOMBINU



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema J. Nchimbi (wa kwanza kushoto) akiwa ofisini kwake alipotembelewa na wajumbe wa Kamati  ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye mkoa huo


Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Willy Quambalo (wa kwanza kulia) akisisitiza jambo kwa wataalamu wa kampuni ya simu ya Halotel wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua
 upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini katika kijiji cha Idondandoye kilichopo wilaya ya Manyoni mkoani Singida. 

Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye maeneo ya vijiji mbalimbali nchi nzima ikiwa ni moja ya jukumu la Kamati hiyo ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya kujenga miundombinu ili kukuza uchumi wa taifa letu, kuchangia pato la taifa na kuiwezesha Serikali kuhudumia wananchi wake.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson Mwkasaka wakiwa kwenye ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasikiano vijijini kwenye  kijiji cha Kijima kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

 Mhe. Mwakasaka amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imwekeza kwenye kampuni ya simu ya Halotel ili iweze kufikisha huduma za mawasiliano vijijini a kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili wananchi wa vijijini waweze kutumia huduma hizo na kunufaika nazo sawa na wanachi waishio mijini.

 Naye Msimamizi wa Kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Benedict Kishusha amesema kuwa Halotel ina watumiaji wachache kwenye vijiji mbalimbali nchini ambako kampuni hiyo imejenga minara na wananchi waishio maeneo hayo wana uwezo mdogo wa kiuchumi wa kutumia huduma za mawasiliano kama vile kununua muda wa maongezi ili kufanikisha azma ya Serikali ya ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini. 

Halotel imekuwa ikiwapatia wananchi simu za mkononi bure bila ya kuwauzia ili waweze kuwasiliana na kutumia huduma nyingine za mawasiliano, amesema Kishusha.

 Ameongeza kuwa kijiji cha Kijima kina takribani ya watu 2,000 na mnara huo umewashwa na kuanza kutumika mwezi Julai mwaka 2015.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka ametoa rai kwa kampuni ya simu ya Halotel kutangaza  huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja na kuweka mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi.

Pia ameongeza kuwa waendelee kujitangaza hasa kwenye maeneo ya vijijini walikojenga minara yao ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano vijijini kama vile kutuma na kupokea fedha kwa kuwa hamna huduma za kibenki kwenye maeneo ya vijijini na wananchi wanategemea huduma hiyo kupitia kampuni ya simu ya Halotel.

 Pia ameongeza kuwa Halotel waendelee kutangaza  huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja na kuweka mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi.

Akizungumza kwenye  ziara hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Kijima wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Ritha Kabati amesema kuwa wananchi wengi wanahitaji huduma ya kuweka na kutoa fedha kwani ndiyo huduma muhimu kwao.

Kabati alisema wananchi wengi walioko vijijini hawatambui kama Haloteli inatoa huduma ya kutoa na kuweka fedha hivyo hutumia mitandao mingine inayopatikana huduma hiyo.

 "Wananchi wengi waliopo vijijini hawatambui kama kuna Halopesa wanachokijua ni M-pesa wakati huduma hii ni muhimu kwa kuwa watoto, ndugu na jamaa walioko mjini huwatumia fedha kwa njia ya simu za mkononi hivyo kukosekana kwa huduma hii kunachangia watu wasiitambue," amesema Rita Kabati.

Pia Mjumbe wa Kamti hiyo Mhe. Mussa Ntimizi alisema serikali imetoa ruzuku kwa kampuni za simu lengo ni kueneza huduma za mawasiliano hivyo baada ya ujenzi wa minara mnatakiwa kuweka promosheni mbalimbali na matangazo ya kutosha kujitangaza. 

"Haloteli  mtengeneze matangazo ya kutosha ili watu waitambue kwani Serikali imeweka fedha za kutosha ili wananchi wapate huduma zote muhimu.

Natambua kwamba huduma ya kuweka na kutoa fedha (Halopesa) imeanza kutoa huduma lakini ipo zaidi mjini hivyo mnapaswa kuitangaza na huku vijijini," alisema Ntimizi. 

Pia amesema kama ambavyo Haloteli inafanya vizuri katika masuala ya data mijini, wanapaswa kuweka huduma hiyo vijijini kwani suala la mawasiliano limekuwa hivyo wasitegemee kuwa wanakijiji hawatumii data.

 "Kwa sasa wananchi wanapendelea zaidi data katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp hivyo msifikiri kwa kuwa huku ni vijijini basi hawatumii hapana, mnatakiwa muweke data nzuri kisha muangalie watumiaji wako wengi kiasi gani," alisisitiza.

Mwanakijiji wa Kijima, Bi. Hellen Michael alisema kuwa katika kijiji hicho wanatumia zaidi mtandao wa Vodacom na kwamba wengi wanatambua huduma za M-Pesa na sio Halopesa.

 Alisema huduma hiyo ya kuweka na kutoa fedha kwa Haloteli imeanza miezi minne iliyopita na kwamba wanakijiji wanapenda kutumia huduma hizo zaidi. 

"Wananchi wanafurahia na kutumia simu ya kampuni ya Halotel bali tunaiomba itoe huduma za kuweka na kutoa pesa".amesema Bi. Hellen Michael.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga amesisitiza kuwa kampuni ya simu ya Halotel itoe huduma za data kwa wananchi waishio vijiji mbalimbali walikojenga minara na sio huduma za simu za sauti tu ili wananchi waweze kupata huduma za mawsilaino ya sauti na data kupitia kampuni hiyo kama ilivyo kwa wananchi waishio mijini.

Msimamizi wa Kampuni ya Haloteli mkoa wa Mwanza na Simiyu, Bwana Benedict Kishusha alisema kuwa mnara huo uliwashwa Julai, 2015  ambao unahudumia vitongoji 23 vya kijiji hicho. Kishusha alisema changamoto mojawapo ni watumiaji wachache wa mitandao ya simu katika kijiji hicho unaosababishwa na uwezo mdogo wa  kupata huduma za mawasiliano ikiwemo ununuaji wa vocha.

 Alisema wanajitahidi kuelimisha watu kutumia mtandao huo ikiwemo kufanya matangazo mbalimbali na kuwapatia bure kadi za simu na muda wa maongezi. "Huduma ya Halopesa imezinduliwa hivi karibuni na kijiji hiki kimeanza kutumia huduma hiyo miezi mitatu iliyopita.  

"Katika mnara huu wanatumia data ya 2G kwani hatuwezi kuweka 3G kwa sababu watumiaji wake ni wachache hivyo  inaongeza gharama," alifafanua Kishusha.

Pia alieleza kuwa awali,  walifunga data ya 3G  lakini kijiji hicho na vingine waliona watumiaji wa simu za mkononi za kutumia data za 3G ni wachache na mfumo wao unasoma hivyo ambapo iliwalazimu kutoa huduma hiyo na kupeleka vijiji vingine na kuacha huduma ya data ya 2G ikiendelea kufanya kazi na kutumika kwenye kijiji hicho.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu, Mhe. Emmanuel Mwakasaka alisisitiza kuwa ni vyema kampuni hiyo kuzingatia kutoa huduma zote ili wananchi waweze kunufaika na  mawasiliano sio tu ya kuongea. 

Pia alizitaka  Kampuni za simu zote zinazotumia huduma za mawasiliano kote nchini kuhakikisha zinashiriki katika kusaidia  huduma za jamii. Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Haloteli mkoa wa Mwanza, Francis Mafuru alisema wanajitahidi kutoa huduma za kijamii licha ya kwamba wananchi hao wapatao 2,000 hawatumii vocha zaidi ya shilingi 500 hali inayoongeza gharama za uendeshaj wa kampuni hiyo ya simu.

 "Tunaamini wateja wetu wataongezeka kwani tumejipanga vizuri kuwahudumia katika masuala ya fedha na data," alisema Mafuru.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Facebook

Wanawake wenye ulemavu wa ngozi kuandika historia mpya kwa kupanda mlima Kilimanjaro.   Mwanaharakati wa haki za binadamu na mp...